Kwa kipindi kirefu sasa suala ya utamaduni wa kujisomea kuwa duni nchini Tanzania limekuwa gumzo na wanazuoni wamelaumu kadambalimbali wakiwemo wanafunzi, waalimu, wasimamizi wa elimu na kadhalika kwa kuwa sehemu ya sababu za tatizo hili.
Hata hivyo, pamoja na sababu nyingi ziwezazo kutolewa moja ambayo imekuwa ikijirudia na inayoonekana kuwa na nguvu ni kukosekana kwa kipaumbele katika mitaala ya elimu yetu katika fasihi. Sera ya elimu nchini inatambua kuwa kujisomea ni njia ya kuongeza maarifa na kukuza uwezo wa lugha (kuandika na kuongea). Hata hivyo, mitaala ya elimu ya msingi, sekondari na sekondari ya juu haitoi kipaumbele kinachostahili ili kushawishi wanafunzi kupenda fasihi.
Ukitizama mtaala wa shule za msingi hauoni ni kwa namna gani watoto wetu wanachochewa kuzifahamu hadithi, ngonjera na mashairi kwa kuwa wabunifu wa kukusanya, kuandika, kusoma/kughani na kuchambua kazi hizi.Ukitizama wenzetu wa Kenya, wanafunzi wa shule za awali wanashiriki kikamilifu katika kusoma kazi za fasihi na kwa kuanzia wanashinikizwa kutoa kipaumbele kwenye kazi ambazo wanaweza kuzipata kwenye mazingira yanayowazunguka.
Kusoma huanza pale mtoto anapoanza kujenga uwezo wa kuelewa mambo na kuyatafiti. Kama waswahili wasemavyo, samaki mkunje angali mbichi ndivyo na watoto wetu wanavyopaswa kukuzwa katika kupenda kusoma. Mtaala wa elimu ya msingi sharti uweke mkazo katika fasihi ili msingi wa kusoma na kuandika ujengwe mapema. Mataala wa elimu ya sekondari nao una mapungufu. Fasihi haina nafasi stahili. Wanafunzi wanatambulishwa katika ulimwengu wa kusoma wakiwa kidato cha pili. Kwa wengi wao kama siyo wote wanaona ni jambo geni kwa kuwa hawana msingi katika fasihi. Kusoma inakuwa ni somo kama fizikia na historia na hakuna msisitizo kuwa kujisomea ni kila wakati. Hali ya kumwandaa mwanafunzi kuamini kuwa kujisomea vitabu vya hadithi ni kwa minajili ya kujibu mtihani huendelea hadi kidato cha 3, 4, 5 na 6 ambapo wanafunzi huelekezwa kujibu maswali hivyo hukariri majibu ya maswali kulingana na hadithi wapaswazo kusoma hata bila ya kuzisoma.
Ndiyo maana wanafunzi wengi wa kitanzania wanaosoma Literature hupenda kusikia kuhusu themes katika kazi ya fasihi kwa kuwa huo ndio msingi wao wa kusoma kazi za fasihi. Mitaala inatoa mwanya kwa wanafunzi kusaka vitini vinavyoandaliwa na watu hivyo kuishia kusoma uchambuzi wao ambao mara nyingi huwa potofu kwa kuwa haulengi hasa kumsaidia mwanafunzi kufahamu fasihi bali kujibu maswali ya NECTA.
Hata ukitizama muhtasari wa masomo ya sekondari na sekondari ya juu utaona kuwa Fasihi imeingizwa kama sehemu tu ya masomo hasa fasihi ya Kiingereza na hufundishwa kama kipengele cha kukamilisha muhtasari. Hata mfumo wa maswali ya NECTA nao unasadifu mfumo huu nilioutaja kwa kuweka maswali ya fasihi katika kipengele kimoja ambapo mwanafunzi hujibu maswali yasiyozidi mawili. Kutokana na hali hii hata ufundishaji wa fasihi hufanywa kama jamno la ziada tu huku msisitizo ukiwa kwenye themes. Wanafunzi wakishakariri wanachokiita themes kwenye kazi watakiwazo kusoma huridhika kuwa wameshafaulu.
Jitihada za makusudi zinahitajika kuondoa hali hii na kuwajengea wanafunzi uwezo wa kusoma na kuandika ili wajijengee uwezo nbinafsi wa kujieleza. Bila kubadili namna mitaala inavyotafsiri fasihi hatuwezi kupiga hatua.
No comments:
Post a Comment